BIG RESULTS NOW : TUNASUBIRI "MATOKEO MAKUBWA SASA" KWENYE RIADHA - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


21 Jul 2014

BIG RESULTS NOW : TUNASUBIRI "MATOKEO MAKUBWA SASA" KWENYE RIADHA


Naibu Waziri wa Habari, Vijana na Michezo, Mhe. Juma Nkamia (wa pili kulia) akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Michezo wa Jumuiya ya Madola leo jijini Glasgow, Uskochi (Scotland). Mkutano huo unafanyika kabla ya ufunguzi rasmi wa michezo ya Jumuiya hiyo, utakaofanyika keshokutwa haoa Glasgow. Agenda kuu ya Mkutano huo ni Michhezo kwa Maendeleo na Amani
Safari hii, serikali kwa kutumia uhusiano wake wa kitamaduni na nchi za China, Uturuki, Ethiopia na New Zealand iliweza kutuma wanamichezo wake kwenye nchi hizo tofauti kulingana na mazingira mazuri ya mchezo fulani ili waweze kujiandaa ipasavyo.
  Na Mwandishi wetu
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo bendera yake itapepea jijini Glasgow, Scotland katika ufunguzi wa Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Julai 23 kwenye Uwanja wa Celtic Perth.

Michezo hiyo muhimu hushirikisha nchi wanachama wa jumuiya hiyo ambazo ziliwahi kuwa koloni la Uingereza na mwaka huu inatarajiwa kushirikisha mataifa 71 ambayo yatachuana katika michezo 17 tofauti itakayofikia tamati Agosti 3.

Katika michezo hii Tanzania inatarajiwa kuwakilishwa na wanamasumbwi, wanariadha, kunyanyua vitu vizito, mpira wa meza, wachezaji judo, waendesha baiskeli na waogeleaji ambao tayari wameshawasili kwenye kijiji cha michezo nchini Scotland tayari kwa michezo hiyo. Katika Michezo ya Madola mwaka huu kuna medali 260 zinawaniwa na tunaamini kati ya hizo Tanzania haitaweza kukosa japo moja kutokana na maandalizi waliyopewa wawakilishi wetu kwenye michezo hiyo.

Watanzania wamechoka kuwa wasindikizaji tena, kama wa harusi, kwenye mashindano ya kimataifa, hivyo mwaka huu matarajio ya wanamichezo wetu kufanya vizuri ni makubwa.

Tunafahamu nchi nyingi zinazoshiriki michezo hiyo zimekuwa na maandalizi kwa wanamichezo wao kwa muda mrefu, lakini hakuna aliyetukataza na sisi kujiandaa kuzidi wao.

Ni ukweli usiopingika kuwa hakuna nchi inayoshinda medali kwa miujiza katika michezo hiyo inayoshirikisha mataifa mengi bali ni maandalizi ambayo tunaamini wanamichezo wetu pia wamefanya vya kutosha. Hivyo Watanzania wanataka kuona wanamichezo wao wanatwaa medali, hawataki kubahatisha au wanamichezo wetu kuishia kushiriki na kurejea kimyakimya.

Msimu huu wa michezo ya 20 ya Jumuiya ya Madola bila shaka ndiyo msimu wanamichezo watakaopeperusha bendera ya taifa wakiwa wameandaliwa ipasavyo tofauti na miaka mingine kama ilivyokuwa 2006 na 2010 wakati Michezo ya Madola ilipofanyika Australia na India ambako wanamichezo wetu hawakupata maandalizi ya kutosha wala kuungwa mkono ipasavyo na wadau, ikiwa ni pamoja na serikalini.

Safari hii, serikali kwa kutumia uhusiano wake wa kitamaduni na nchi za China, Uturuki, Ethiopia na New Zealand iliweza kutuma wanamichezo wake kwenye nchi hizo tofauti kulingana na mazingira mazuri ya mchezo fulani ili waweze kujiandaa ipasavyo.

Hivyo, tunachokitarajia msimu huu ni medali kwa wanamichezo wetu 39 waliopo Scotland kwani kwa kufanya hivyo watarejesha matumaini kwa Watanzania kuendelea kuiunga mkono timu yao inapokwenda kwenye mashindano makubwa.

Tanzania ina historia na Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa kuwa ndiyo iliyowezesha nchi hii kuvunja medali ya kwanza ya dunia ya mbio za mita 1,500.

Ni matumaini yetu kuwa wanamichezo wetu watakuwa na hilo akilini mwao kuwa wanao wajibu wa kuendeleza historia hiyo kwa kufanya vizuri zaidi na ikiwezekana kuweka rekodi za dunia.

Tunaamini maandalizi waliyoyapata kwenye nchi hizo yamewaweka vizuri kimchezo na kisaiokolojia na hivyo kilichobakia ni “Matokeo Makubwa Sasa”.

CHANZO: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad