ELIMU YETU :MAMA ASHA IDDI AHUDHURIA HAFLA YA KUAGWA WANAJUMUIYA WANAOHITIMU MASOMO YAO KWA 2014 - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


18 Aug 2014

ELIMU YETU :MAMA ASHA IDDI AHUDHURIA HAFLA YA KUAGWA WANAJUMUIYA WANAOHITIMU MASOMO YAO KWA 2014


 Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo kikuu cha Kiislamu Morogoro Nd.Kassimu N’gwali akitoa neno la shukrani kwa waalikwa wa hafla yao ya kuagana kwa wanajumiya wanaomaliza masomo yao mwezi Septemba mwaka huu wa 2014. Kushoto ni Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae ndie mgeni rasmi wa hafla hiyo Mama Asha Suleiman Iddi.
 Baadhi ya wana jumuiya ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro wakifuatilia hafla ya maagano kwa wanajumiya wanaotarajiwa kumaliza mafunzo yao mwezi Septemba mwaka huu.
 Mwanajumiya ya ZAMUMSA Saleh Haji alitaja baadhi ya changa moto wanazopakabiliana  nazo wakati akisoma Risala ya jumiya hiyo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa ZAMUMSA Bibi Saada akimkabidhi zawadi Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi kwenye hafla ya kuagana wanajumiiya hiyo wanaomaliza masomo yao mwezi Septemba mwaka huu.
 Mama Asha Suleiman Iddi akizungumza na Wana Jumuiya ya ZAMUMSA kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mama Asha akimkabidhi Cheti Maalum Mwenyekiti mstaafu wa ZAMUMSA Nd. Rashid Mjaka kwa niaba ya viongozi wenzake baada ya kumaliza muda wao wa utumishi wa jumuiya hiyo. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
**********************************
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema kwamba utitiri wa vyuo vikuu bila ya ubora wa elimu inayotolewa ni jambo linalopelekea vyuo hivyo kutoa vijana wasiouzika kiajira katika taasisi mbali mbali za umma na hata zile za binafsi.
Alisema athari hiyo ambayo pia ni hatari kwa hatma yao ya kimaisha hapo baadaye pia inaweza kuwanyima fursa pana nay a uhakika ya kujiunga na vyuo vyengine vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi.
Mama Asha Suleiman Iddi  alisema hayo wakati wa hafla maalum ya kuagana kwa wana jumuiya ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro wa  ZAMUMSA ambao wanatarajiwa kumaliza mafunzo yao mwezi Novemba mwaka huu.
Hafla hiyo ya aina yake iliyoshirikisha pia baadhi ya wahitimu wengine wa vyuo vikuu mbali mbali Nchini Tanzania ilifanyika katika ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mama Asha alisema vyuo  vikuu viliopo hapa nchini hivi sasa  vinatosha, lakini kinachohitajika zaidi ni kuimarishwa kwa ubora wa elimu inayotolewa kwenye vyuo hivyo.
Aliwataka wasomi wa vyuo vikuu wanaomaliza masomo yao kuweka malengo maalum ya kujiendeleza kimaisha ili kuwa tayari kukabiliana na changamoto watakazokuja pambana nazo katika maisha yao ya baadaye.
Alisema Zanzibar ni ndogo kulingana na wimbi la vijana wanaomaliza elimu ya vyuo vikuu. Hivyo akasema ni vyema wakajiandalia mazingira ya kujiunga katika vikundi vya uzalishaji ndani na nje ya vyuo ili kuwa tayari katika kukabiliana na matatizo ya kimaisha wamalizapo masomo yao.
Mama Asha alifahamisha kwamba jumuiya ya ZAMUMSA  inafaa kufanya miradi ya kisomi kwa kutengeneza vitini na kuwauzia wanafunzi wa sekondari na pale inapowezekana hata kutunga vitabu vya sekondari katika masomo mbali mbali.
Katika kuunga mkono jumuiya hiyo ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo kikuu cha Kiislamu Mkoani Morogoro Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha aliahidi kuipatia mchango wa Kompyuta, Printa na Mashine ya Fotokopi Jumuiya hiyo ili ipate nguvu zaidi za kiutendaji.
Hata hivyo Mama Asha aliwaasa na kuwatahadharisha wanafunzi hao wa elimu ya juu kujiepusha na ushawishi wa wanasiasa kwa kuwatumia kujiingiza katika matendo maovu ya uvunjifu wa amani ya Nchi.
Alisema wasomi mara nyingi ndio wanaotumiwa katika kufanya fujo na kuvuruga amani katika maeneo mbali mbali duniani kupitia mkono wa Viongozi wa kisiasa.
Akigusia suala la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu kulazimishwa kusomea fani wasiyoitaka, mama Asha alisema suala hilo bado linazungumzika  bila ya kuleta utata au hofu yoyote ile.
Alitoa wazo kwa wana jumuiya hiyo pamoja na wasomi wengine  kukutana na Uongozi wa juu wa Wizara inayoshughulikia Taaluma katika kutafuta njia muwafaka ya kulitatua  tatizo hilo kwa njia sahihi isiyo na shaka.
Akisoma risala ya wanajumuiya hiyo ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma Chuo Kikuu cha Kiislamu Mkoani Morogoro { ZAMUMSA } Mwanajumuiya Saleh Haji alisema lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo mwaka 2006 ni kuwaunganisha pamoja wanafunzi wote ili kuwa rahisi kukabiliana na changamoto wanazopambana nazo.
Saleh Haji kwa niaba ya wanajumiya wenzake wameiomba Serikali Kuu kuongeza nguvu za ziada katika uimarishaji wa maabara na Maktaba kwa skuli za Sekondari ili kuzalisha wanafunzi wa sayansi ambao hivi sasa bado idadi yao hailingani na mahitaji halisi ya upatikanaji wa wataalamu wa fani hiyo.
Aidha wanafunzi hao wa ZAMUMSA wameiomba Serikali kufanya juhudi ya kuwadhibiti wasomi wanaomaliza elimu ya juu kwa kuwajengea mazingira mazuri yatakayowapa hamu ya kuitumikia elimu yao hapa nyumbani.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro Hamad Ali alisema wanajumiya hao wameamua kujitolea kuitumikia nchi yao licha ya changamoto wanazopambana nazo.
Hamad Ali alisema wanafunzi hao wanahitaji kuitumia taaluma waliyojifunza kwa kuisaidia jamii iliyowazunguuka katika maeneo yao.
Wanafunzi wasiopungua mia 800 kutoka Zanzibar wamejiunga na chuo kikuu cha Kiislamu Morogoro katika fani mbali mbali ikiwa ni zaidi ya asilimia 47% ya wanafunzi wote chuoni hapo.
Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na vyuo vyengine vikuu hapa Tanzania inayotokana na mazingira halizi ya chuo hicho yanayolingana na utamaduni na silka za wanafunzi hao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad