MAENDELEO YETU :SERIKALI KUWASHIRIKISHA VIJANA KATIKA PROGRAMU ZA MAENDELEO - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


18 Aug 2014

MAENDELEO YETU :SERIKALI KUWASHIRIKISHA VIJANA KATIKA PROGRAMU ZA MAENDELEO


DSC_0069
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA), Dkt Natalia Kanem akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ya siku ya kimataifa ya vijana duniani kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kushoto ni Mgeni Rasmi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bibi Venerose Mtenga na kulia ni Mtaalamu wa Programu za Vijana kutoka UNFPA, Tausi Hassan.( Picha na Zainul Mzige wa MOblog).
.Siku ya vijana duniani na ujumbe wa “Vijana na Afya ya Akili”
.Takwimu zinaonyesha nusu ya idadi ya watu nchini ni vijana

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI Kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo imeahidi kukuza na kuboresha misingi ya kuwashirikisha vijana katika utekelezaji wa sera mbalimbali, programu na mikakati ya maendeleo.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bibi Sihaba Nkinga, wakati wa maadhimisho ya siku ya vijana duniani kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bibi Venerose Mtenga amesema kwamba lengo la kuwashirikisha vijan ni kuhakikisha kuwa sauti zao zinasikika na kufanyiwa kazi.
“Katika kutekeleza eneo hili Tanzania inalenga kuweka fursa zitakazowawezesha vijana kukuza utaalamu na ujuzi utakaowawezesha kufanikiwa katika kipindi cha mpito kutoka ujana kwenda katika utu mzima,” amesema Bibi Mtenga.
Amesema kwamba Tanzania kama sehemu ya dunia inatambua changamoto maalum zinazowakabili vijana walioko katika mazingira hatarishi pamoja na umuhimu wa kuhakikisha kuwa vijana wanahusishwa kikamilifu katika malengo ya maendeleo.
DSC_0096
Bi Mtenga aliongeza Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na vijana pamoja na wadau wa maendeleo ili kuunga mkono programu za elimu ya afya kwa vijana walioko ndani na nje ya shule.
Alilisitiza kwamba Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo wataendelea kuunga mkono taasisi za mafunzo rasmi na zisizo rasmi ili kukuza uwezo na uelewa miongoni mwao katika masuala ya afya ya akili na mwili kwa ujumla.
“siku ya vijana duniani inatambua na kuthamini kuwa kipindi cha ujana kinaambatana na mabadiliko makubwa na ya haraka na safari ya kutoka utotoni kufikia utu mzima,”
“Safari hiyo inaweza kuwa ngumu na yenye changamoto nyingi na hivyo kuhitaji utulivu na ukomavu wa akili, hapa Tanzania, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya vijana, kijana ni mtu yeyote mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 35,” aliongeza
Amesema kwamba katika takwimu za kitaifa hapa nchini nusu ya idadi ya watu ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa na uchumi wa nchi kwa ujumla.
DSC_0133
Mgeni Rasmi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bibi Venerose Mtenga akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ya siku ya kimataifa ya vijana duniani, kushoto kwake, ni Mwakilishi wa UNFPA, Dkt. Natalia Kanem.
Bibi Mtenga aliendelea kusema kwamba msisitizo mkubwa unawekwa katika kuhakikisha vijana wanakuwa na fikra chanya ambazo ni za kimaendeleo na zinazoleta mabadiliko chanya kwa jamii.
Kwa Upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA), Dkt. Natalia Kanem amesema kwamba siku ya vijana duniani ni nafasi nyingine kwa vijana kukutana pamoja na kujadiliana matatizo na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Amesema kwamba vijana kwa kushirikiana na makundi mbalimbali ya kitaifa na kimataifa katika kupambana na changamoto za matumizi ya pombe kupita kiasi, dawa za kulevya na mimba za utotoni.
“kwa pamoja serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kimataifa wana wajibu wa kushirikiana na vijana katika kuwasaidia kufikia malengo yao mbalimbali katika harakati za kujiletea maendeleo,” amesema Dkt. Kanem.
DSC_0041
Baadhi ya timu za mpira wa kikapu na wanafunzi kutoka shule mbalimbali za sekondari nchini wakimsikiliza mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani.
Dkt Kanem aliongeza kwamba ni muhimu kwa vijana kutambua kwamba bila kuwa na afya nzuri ya akili ni vigumu kupiga hatua za kimaendeleo na kuondokana na umaskini wa kipato.
Amesema kwamba katika mkutano unaokuja wa viongozi duniani watatumia nafasi hiyo kuwakumbusha viongozi wa dunia umuhimu wa kuwekeza kwa vijana kama taifa la kesho.
Dkt.Kanem alifafanua umuhimu wa vijana na jamiii kwa ujumla kutumia mitandao ya kijamii katika kupashana habari za afya ya uzazi na mambo yanayowahusu vijana kwa ujumla.
Wakati huo huo, Katika mashindano ya mpira wa kikapu timu zilizoshiriki ni timu saba kati ya hizo tano ni za wanaume na pili za wasichana.
DSC_0061
Kwa upande wa wasichana mshindi wa kwanza ni Don Bosco Lioness na washindi wa pili ni Tanzania Prisons Queens na kwa upande wa wavulana, washindi wa kwanza Lord Baden-Powell Memorial High School, washindi wa pili Makongo High School, washindi wa tatu ni Kizuka Sekondari school.
Timu zilizoshiriki ni Tanzania Prisons Queens, Lord Baden-Powell Memorial High School, Makongo High School, Don Bosco Lioness, Kizuka Sekondari School, Tabata Segerea na Bahari Beach.
DSC_0157
Mgeni rasmi, Venerose Mtenga akirusha mpira wa kikapu kuzindua rasmi mashindano ya mchezo wa mpira wa kikapu kwa vijana wa shule za sekondari nchini wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani.
DSC_0150
Mwakilishi wa UNFPA, Dkt Natalia Kanem akirusha mpira wa kikapu kuashiria uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani.
DSC_0161
Mgeni Rasmi na Mwakilishi wa UNFPA wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya timu za mpira wa kikapu.
DSC_0183
Mgeni rasmi, Venerose Mtenga akiwa katika picha ya pamoja na timu ya wasichana ya mpira wa kikapu wakati wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana duniani.
DSC_0175
Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama (kulia) na Mgeni rasmi, Venerose Mtenga (kushoto) wakimuonyesha jambo Mwakilishi wa UNFPA, Dkt Natalia Kanem (katikati) mara baada ya kupata picha za kumbukumbu na timu zilizoshiriki bonanza hilo la mpira wa kikapu katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana duniani.
DSC_0201
Mwakilishi wa UNFPA, Dkt Natalia Kanem akisalimiana na msanii muziki wa bongo flava Domokaya (wa pili kulia) wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani.
DSC_0636
Mtaalam wa Mawasiliano kutoka UNFPA, Sawiche Wamunza akipata u-selfie na msanii wa bongo flava Domokaya wakati wa maadhimisho hayo.
DSC_0639
Phillip Musiba kutoka kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) akipata picha na msanii wa muziki wa bongo flava nchini Domokaya.
DSC_0228
Timu za Kizuka sekondari kutoka Morogoro, (Nyeupe) na Makongo Sekondari (Njano) wakitoana jasho katika mchezo wa ufunguzi wa mpira wa kikapu, Makongo walishinda vikapu 30 dhidi ya 14 ya Kizuka sekondari kutoka Morogoro.
DSC_0235
DSC_0245
Mgeni Rasmi, Bibi Venerose Mtenga akifafanuliwa jambo kutoka kwa Mshauri wa vijana, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNNFPA), Bw, John Kalimwabo alipotembelea banda hilo.
DSC_0271
Mgeni Rasmi, Bibi Venerose Mtenga akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwalimu Tatu Mwakifuna na Mwanafunzi wake, Zawadi Salehe wote kutoka KIWOHEDE. Kushoto kwa mgeni rasmi ni Mtaalamu wa Programu za Vijana kutoka UNFPA, Tausi Hassan.
DSC_0294
Mgeni rasmi akipata maelezo kutoka kwenye banda la Tanzania Network Against Alcohol Abuse kwenye moja la shirika lake la Tanzania Girl Guides Association, anayetoa maelezo ni Fadhia Khamis Ally na kushoto kwake ni Shadya Soud Milanzi wasichana hao wanatoka Girl Guides ambacho ni chama kisicho cha kiserikali na ni chama cha kujitolea, madhumuni yake ni kuwaendeleza wanawake pamoja na motto wa kike katika maswala ya kijamii na kiuchumi kwa kuwapa elimu na mafunzo.
DSC_0304
Mgeni rasmi, Bibi Venerose Mtenga akimsikiliza kijana kutoka Kituo cha Vijana UMATI, Temeke, Kassim Abdallah alikuwa akimweleza mgeni rasmi jinsi wanavyotoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana kwa kutumia vipeperushi na ushauri nasaha.
DSC_0343
Wawakilishi kutoka Marie Stopes Hospital Tanzania, Bibi Zayana Nuhu na John Basso Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wakimweleza jambo mgeni rasmi jinsi hospitali hiyo inavyofanya kazi hapa nchini.
DSC_0352
Mgeni rasmi akipata picha ya kumbukumbu na mmoja wa wahudumu wa banda la Marie Stopes wakati wa maadhimisho hayo.
DSC_0518
Joynes Ashery kutoka Marie Stopes Hospital Tanzania akifafanua jambo kuhusiana na masuala ya afya ya uzazi kwa Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) ambao ni wameshiriki kuratibu maadhimisho hayo, Stella Vuzo.
DSC_0392
Mshauri wa vijana, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNNFPA), Bw, John Kalimwabo akitoa maelezo ya matumizi sahihi ya Kondomu za kike kwa kutumia kiungo bandia cha mwanamke kwa vijana waliohudhuria maadhimisho ya kimataifa ya siku ya vijana duniani.
DSC_0398
Vijana wakiendelea kumiminika kwenye banda ya UNFPA kupata maelezo mbalimbali wakati wa maadhimisho ya kimataifa ya siku ya vijana duniani yaliyofanyika mwishoni mwa juma kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
DSC_0489
Mratibu wa uzazi wa mpango kutoka shirika la PSI, Hadija Ameir akitoa elimu ya uzazi wa mpango kwa vijana wakati wa maadhimisho hayo katika viwanja vya Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.
DSC_0545
Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Stella Vuzo akizungumza na baadhi ya watoto walioshiriki mashindano ya kuchora picha mbalimbali zikiwemo za kuhamasisha vijana kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya baada ya kuvutiwa na kazi zao.
DSC_0549
Mtoto Tarzan Iddy akionyesha picha yake aliyoichora ikizungumzia uvutaji wa Bangi kwa vijana.
DSC_0738
Mgeni rasmi, Bibi Venerose Mtenga na Afisa Habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama wakikagua baadhi ya picha hizo na maudhui kabla ya kutangaza washindi.
DSC_0742
DSC_0755   
Mgeni rasmi, Bibi Venerose Mtenga akikabidhi nyenzo za sanaa ya uchoraji zilizotolewa na UNFPA kwa mtoto Lawrence Dennis wakati wa maadhimisho ya kimataifa ya siku ya vijana duniani.
DSC_0765
Mgeni ramsi Bibi Venerose Mtenga akimkbidhi mmoja kati ya tatu bora wa mashindano ya uchoraji Aziza Iddy nyenzo za sanaa ya uchoraji kutoka kwa zilizotolewa na UNFPA sambamba na ufadhili wa kusomeshwa kulipiwa ada ya darasa la uchoraji kwa siku tano.
DSC_0835
Mgeni ramsi Bibi Venerose Mtenga akiwavalisha medali timu zilizochukua ubingwa wakati wa maadhimisho hayo.
DSC_0801
Mgeni ramsi Bibi Venerose Mtenga akimkabidhi zawadi Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) Michael Maluwe kama shukrani ya kuratibu bonanza la mpira wa kikapu kwa vijana wakati wa maadhimisho hayo.
DSC_0944
Mgeni ramsi Bibi Venerose Mtenga akiwa kwenye picha ya pamoja na washindi wa kwanza wa bonanza la mpira wa kikapu timu ya Lord Baden-Powell.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad