MATUKIO : LUKUVI AZOMEWA MBELE YA RAIS JAKAYA KIKWETE, DODOMA - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


3 Sept 2014

MATUKIO : LUKUVI AZOMEWA MBELE YA RAIS JAKAYA KIKWETE, DODOMA

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amejikuta katika wakati mgumu mbele ya Rais Jakaya Kikwete baada ya kuzomewa hadi kukatisha hotuba yake akipingwa na wananchi pamoja na madiwani wa CCM wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma alipokuwa akitetea kuwapo kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
Lukuvi alikumbana na mkasa huo wakati akijibu hoja za Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), David Malole ambaye alitaka CDA ivunjwe akiituhumu kuwavunjia wananchi nyumba bila kuwatafutia mahali pa kuishi.
Hoja ya Malole kutaka CDA ivunjwe iliibuka katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kikuyu, Manispaa ya Dodoma baada ya Rais Kikwete kuzindua ujenzi wa Barabara ya Dodoma - Iringa.
Awali, mbunge huyo akitoa salamu kwa Rais Kikwete, alisema CDA imekuwa ni kero kwa wakazi wa mji huu.
“Mheshimiwa Rais, ni bora CDA ikafutwa na ardhi ikarudishwa kwa halmashauri kwa kuwa hakuna kitu kinachofanyika. Ipo miji mingi ambayo haina CDA lakini imekuwa majiji. Leo hii zaidi ya miaka 40 CDA imeshindwa kuufanya Mji wa Dodoma kuwa jiji,” alisema na kuongeza:
“Licha ya kuwa CDA jukumu lake ni kuhakikisha inapima viwanja na kupanga ustawi wa mji lakini imeshindwa kufanya hivyo, jambo ambalo linawakera wananchi wa Dodoma na kusababisha kukichukia Chama Cha Mapinduzi na Serikali yao,” alisema.
Kutokana na hoja hiyo kushangiliwa na madiwani pamoja na wana CCM na wananchi wengine, Malole aliendelea kufafanua kuwa suala la kupigania wananchi wapate viwanja linamuweka katika hali ngumu kwa sababu anatishiwa kuwa hatapata nafasi ya kugombea ubunge tena.
“Mimi nasema, ikimpendeza Mungu kuwa mbunge nitaendelea kuwa mbunge na kama siyo mpango wa Mungu basi, kwani kuna propaganda nyingi juu yangu lakini hiyo yote ni kutokana na kupigania wananchi wapewe haki zao,” alisema.

Kuzomewa
Baada Malole kutoa madai hayo, Lukuvi ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya CDA alilazimika kupanda jukwaani ili asawazishe kauli za mbunge huyo, jambo ambalo liliibua zogo na wananchi kuzomea.
Zomeazomea dhidi ya Lukuvi ilitawala katika kipindi chote alichokuwa jukwaani huku viongozi wa chama wakihaha kuwazuia wanachama na madiwani wa CCM wasizomee bila mafanikio.
Hali iliendelea kuwa mbaya kwa Lukuvi pale aliposema, “Mimi ni mdau mkubwa wa CDA na ni kati ya watu ambao walishiriki kupeleka maendeleo katika Mji wa Dodoma.”
Kauli hiyo ilisababisha madiwani pamoja na wananchi kuanza upya kumzomea huku wakimtaka ashuke jukwaani kwa madai kuwa hana cha kuwaeleza hadi wamwelewe.
Hali hiyo iliambatana na nyimbo zilizoanzishwa na madiwani, “CCM.. shuka chini, CCM shuka chini” hali iliyomfanya Lukuvi kushuka jukwaani.
Baadaye Rais Kikwete akizungumza na wakazi hao, alitoa siku saba kwa viongozi wa mkoa kwa kushirikiana na mbunge kukaa na kutatua mgogoro huo na aliahidi kukutana nao Septemba 8, mwaka huu.
Alisema migogoro haiwezi kutatuliwa katika mikutano ya hadhara, bali vikao vya kazi. Aliwataka kukutana kuangalia ni jinsi gani watamaliza mgogoro huo bila kuwa na fujo wala lawama.
Chanzo :MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad