MATUKIO : TAASISI 13 ZILIZOKAGULIWA NA PPRA ZAGUNDULIKA KUWA NA VIASHIRIA VYA RUSHWA KATIKA UNUNUZI - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


8 Oct 2014

MATUKIO : TAASISI 13 ZILIZOKAGULIWA NA PPRA ZAGUNDULIKA KUWA NA VIASHIRIA VYA RUSHWA KATIKA UNUNUZI


 Mwenyekiti wa Mamlaka  ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dk. Martern Lumbanga (kushoto), akizungumza katika mkutano  na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu matokeo ya ukaguzi wa shughuli za ununuzi katika taasisi za umma uliofanywa na PPRA kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 mwaka huu. Kulia ni Mjumbe wa Bodi ya PPRA, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo.
 Mjumbe wa Bodi ya PPRA, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo akizungumza katika mkutano huo. 
 Wajumbe wa Bodi wakiwa kwenye mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mhandisi Leonard Chamuriho, Profesa Silvia Temu na Mhandisi Boniface Muhegi.
 Maofisa mbalimbali wa Sekretarieti ya PPRA wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.

Na Dotto Mwaibale

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), imesema taasisi 13 ilizozikagua manunuzi yake yalikuwa na viashiria vya rushwa.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Dk. Martern Lumbanga wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu matokeo ya ukaguzi wa shughuli za ununuzi katika taasisi za umma uliofanywa na PPRA kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 mwaka huu.

"Taasisi hizo zilionekana kuwa na viwango vya zaidi ya asilimia 20 ya viashiria vya rushwa" alisema Lumbaga.

Lumbanga alizitaja taasisi hizo kuwa ni Halmshauri ya Wilaya ya Kondoa, Kilwa, Kishapu, Monduli, Maswa, Mamlaka ya Maji na Mazingira Lindi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Ofisi ya Katibu Tawala ya Mkoa wa Lindi.

Alitaja taasisi zingine kuwa ni Halmshauri ya jiji la Mwanza, Halmshauri ya jiji la Dar es Salaam, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Halmshauri ya Manispaa ya Musoma na Halmshauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Alisema hatua iliyofikiwa na PPRA kwa taasisi hizo ni kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) ili kufanya uchunguzi zaidi na kuchukua hatua kwa taasisi hizo.

Katika hatua nyingine PPRA imezifungia kampuni 19 kushiriki zabuni kwenye taasisi za umma nchini kutokana na kushindwa kutekeleza kikamilifu mikataba zilizoingia na taasisi za umma na hivyo kusababisha mikataba hiyo kuvunjwa.

Alisema Bodi ya PPRA imezisimamisha kampuni nne kushiriki katika zabuni za umma kwa muda mpaka pale mchakato wa kuzifungia au la utakapofikiwa.



Lumbanga alizitaja  taasisi zilizofanya vibaya katika manunuzi ya umma kuwa ni Mamlaka ya Maji  na Mazingira Lindi (Uwasa), Halmsahauri ya Wilaya ya Kishapu, Kibondo, Kilindi, Lushoto na  Ofisi ya Katibu Tawala ya Mkoa wa Lindi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad