Elimu Yetu : Mahafali ya 49 Chuo cha CBE Yafana, Serikali yayataka Makampuni kuacha kutoa nafasi nyingi za Ajira kwa Wageni - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


17 Nov 2014

Elimu Yetu : Mahafali ya 49 Chuo cha CBE Yafana, Serikali yayataka Makampuni kuacha kutoa nafasi nyingi za Ajira kwa Wageni


Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah Kigoda (kulia) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 49 ya Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam akiimba wimbo wa Taifa wakati wa ufunguzi rasmi wa mahafali hayo jijini Dar es salaam. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Mathew Luhanga (katikati) na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Emanuel Mjema.
Baadhi ya wahitimu wa shahada ya Uhasibu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam mwaka 2014 wakisubiri kutunukiwa shahada zao wakati wa mahafali ya 49 yaliyofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl,Ubungo jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Emanuel Mjema akizungumza na wahitimu 3459 wa fani mbalimbali wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam waliohitimu masomo yao mwaka 2014.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)Prof. Mathew Luhanga akizungumza na wahitimu hao.
Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es salaam wakiwa na nyuso za furaha wakati wa mahafari ya 49 ya chuo hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl jana jijini Dar es salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah Kigoda akisoma tamko la kuwatunuku wahitimu 3495 wa fani mbalimbali wa chuo cha CBE wakati wa mahafali ya 49 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah Kigoda akiondoka ukumbini akiwa ameambatana na viongozi wengine wa chuo cha Elimu ya Biashara CBE kampasi ya Dar es salaam mara baada ya kufunga rasmi mahafali hayo. Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.

Na. Aron Msigwa – Dar es salaam.

SERIKALI imewataka watendaji na wamiliki wa makampuni mbalimbali kutoka ndani na  nje nchi  kuacha tabia ya kutoa nafasi nyingi za ajira kwa wageni na badala yake wawatumie vijana wa kitanzania wanaohitimu masomo  katika vyuo mbalimbali  hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es salaam na Waziri wa Viwanda Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda wakati akizungumza na wahitimu 3363 wa fani mbalimbali wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya  Dar es salaam waliohudhuria mahafali ya 49 ya  chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es salaam. 

Amesema Tanzania ina vijana wengi wenye kukidhi viwango na uwezo wa kutekeleza majukumu ya Uhasibu,Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko,Manunuzi na Ugavi , Mizani na Vipimo pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ufanisi mkubwa kutokana na mafunzo waliyopewa katika vyuo na taasisi mbalimbali  hapa nchini.

 “Tanzania tunao vijana bora na wenye kukidhi viwango wanaohitimu kila mwaka,suala la kutoa visingizio  kuwa hatuna wataalam na makampuni haya kuajiri wageni katika nafasi za kawaida na ngazi za utawala mimi sikubaliani nalo ,nakemea tabia hii”  Amesisitiza Dkt. Kigoda.

Amefafanua kuwa Serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ukosefu wa ajira lililopo hapa nchini kwa kujenga na kuandaa mazingira wezeshi ya kukuza utengenezaji wa ajira za kujiajiri na kuajiriwa kwa kuendeleza sekta binafsi katika eneo la Kilimo, Sekta ya Viwanda na Biashara hususan ujasiriamali mdogo na wa kati.

Ameeleza kuwa serikali inaendelea kujenga mazingira wezeshi na rafiki kwa wahitimu hao kujiajiri wenyewe kwa kuratibu mfumo wake wa kodi na tozo mbalimbali, kuangalia hatua za utoaji wa leseni na usajili wa biashara, kushughulikia tatizo la uhaba wa mikopo na riba zinazotolewa kwa wale wanaotumia mikopo kama mitaji pamoja na kushughulikia suala la mikataba inayoandaliwa na makampuni ambayo mara nyingi inawakosesha vijana fursa ya kupata ajira.

Ametoa wito kwa wahitimu hao kuwa wajasiri na wenye moyo wa kuthubutu wa kutumia taaluma na mafunzo waliyopata kuleta mabadiliko na maendeleo nchini huku akiwataka wahitimu hao kuepuka tabia ya uzembe, uvivu na Rushwa pindi watakapoingia kwenye ajira.

Kuhusu uboreshaji chuo hicho Dkt. Kigoda amesema Serikali inaendelea kukijengea uwezo chuo hicho kwa kuimarisha ubora wa mafunzo yanayotolewa hususan matumizi ya mifumo ya kompyuta na mawasiliano (ICT) ili kiweze kushindana na vyuo vya kigeni vilivyoanzisha kampasi zao hapa nchini.

Kwa upande wake  mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho Prof. Mathew Luhanga akizungumzia   mahafali hayo ya 49 ya chuo hicho amesema kuwa yanakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho.

Amesema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965 mafanikio mbalimbali yamepatikana yakiwemo ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kujiunga na masomo hadi kufikia kutoka 25 pindi chuo kinaanzishwa hadi 14000 wa sasa, ongezeko la kampasi kutoka 1 hadi kufikia 4.

Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo kutoka 1iliyokuwepo mwaka 1965 hadi 6 zilizopo sasa na ongezeko la wakufunzi wenye shahada ya uzamivu (PhD).

 Prof. Luhanga amefafanua kuwa chuo hicho sasa kimeanzisha ushirikiano wa elimu na vyuo vikuu vingine  vilivyo nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Maastricht cha Uholanzi, Chuo Kikuu cha Stockholm cha Sweeden na Chuo Kikuu cha Eastern Finland ambacho kimeshirikiana na CBE  kutoa mafunzo ya shahada ya uzamivu  kwa nchi za SADC.

Naye Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema akiwakaribisha wahitimu, wadau mbalimbali na Wanajumuiya wa Chuo hicho waliohudhuria  mahafali hayo  amesema  kuwa chuo chake kimepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965 ikiwemo ongezeko la idadi ya wanafunzi wa kike wanaohitimu chuoni hapo hadi kufikia asilimia 48 kwa mwaka 2014.

Amesema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho wataalam wengi katika fani za Uhasibu,Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko,Manunuzi na Ugavi , Mizani na Vipimo pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wameweza kuhitimu na kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad