Ajira Mpya ya Waalimu 2015 : Ajira za Walimu wa Cheti (Shule za Msingi) 2015 Ziko Hapa, Sekondari Msubiri Kidogo - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


28 Apr 2015

Ajira Mpya ya Waalimu 2015 : Ajira za Walimu wa Cheti (Shule za Msingi) 2015 Ziko Hapa, Sekondari Msubiri Kidogo









Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini (kulia) akizungumza jambo.


Dar es Salaam.

Serikali imetangaza ajira mpya za walimu 31,056 wanaotakiwa kuanza kazi kuanzia Mei Mosi, mwaka huu.
Mbali na walimu, pia imetangaza ajira kwa mafundi sanifu wa maabara 10,625 ambao pia wataanza kazi sambamba na walimu hao.Akizungumza jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini alisema Serikali imetenga Sh9 bilioni kwa ajili ya posho za kujikimu na nauli kwa walimu na mafundi sanifu maabara.

Alisema kiasi cha fedha kilichotengwa ni posho ya siku saba na fedha za nauli ambazo zinatakiwa kulipwa na halmashauri ambazo ndiyo mwajiri.

Alisema posho hizo zinatakiwa kulipwa ndani ya siku saba na kwamba isizidi siku 14 tangu kuripoti kwa mwalimu katika kituo cha kazi.

“Hatutapenda kusikia malalamiko kutoka kwa walimu hao, halmashauri zijipange kuwapokea waajiriwa wao wapya,” alisema.

Mwaka jana kulikuwa na malalamiko ya baadhi ya walimu wapya ambao licha ya kuripoti kwenye vituo vya kazi, walicheleweshewa posho za kujikimu na nauli.

Alisema idadi hiyo ya watakaoajiriwa inajumuisha walimu 11,795 wa ngazi ya cheti, 6,596 wa stashahada na 12,666 wa shahada.

Alisema walimu 2,700 wa masomo ya sayansi na hisabati wamepangwa moja kwa moja kwenye shule ambazo hazina walimu wa masomo hayo.

“Tofauti na walimu hawa wa sayansi waliopangiwa moja kwa moja kwenye shule zisizo na walimu, walimu wa masomo ya sanaa, kilimo, michezo na elimu maalumu watapangiwa vituo vya kazi na halmashauri,” alisema.

“Walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ni wachache ndiyo maana tumeamua kuwapangia moja kwa moja kwenye vituo ili kuhakikisha kila shule inakuwa na walimu wa hisabati baiolojia, fizikia na kemia,” alisema.

Sagini alisema ajira za walimu kwa mwaka huu zimeelekezwa zaidi katika halmashauri zenye uhaba mkubwa wa walimu ili kuweka uwiano sawa na bora wa mwalimu na mwanafunzi kitaifa.
“Kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora iliyokuwa na uwiano mwalimu mmoja kwa wanafunzi 211, wamepelekewa walimu 1,143 ili kufanya shule ziwe na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45 ambao ndiyo wastani unaoelekezwa na sera ya elimu.”

Alisema kuna halmashauri hasa zilizoko mijini ambazo hazikupangiwa walimu mwaka huu kwa sababu zina idadi inayojitosheleza.

Alizitaka halmashauri ambazo ndiyo waajiri, kupanga walimu na mafundi sanifu wa maabara bila ya upendeleo ili kila shule iweze kuwa na walimu wa kutosha na kuweka utaratibu mzuri wa kuwapokea watumishi hao wapya.

Sagini alisema mbali na posho za kujikimu, watatakiwa kurudishiwa nauli walizotumia kutoka makwao kwenda kwenye halmashauri walizopangiwa.

Alisema nauli watakazorudishiwa ni za basi au treni za daraja la kawaida.

Pia watatakiwa kujiunga katika mifuko ya hifadhi ya jamii wanayoipenda bila kupata ushawishi usio wa kawaida kutoka kwa mwajiri.

Alisema ili kuepuka watumishi wapya kukosa mshahara wa mwezi wa kwanza baada ya kuajiriwa, watumishi hao wametakiwa kuripoti kituo cha kazi kabla ya Mei 9 na kwamba kinyume chake mtumishi atalipwa malimbikizo ya mshahara wa kwanza.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad